Wednesday, May 7, 2014

Vibarua Strabag wakwamisha kazi tena




Dar es salaam. Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi  ya Strabag wamegoma na kusimamisha shughuli zote za kampuni hiyo kwa saa tisa, kutokana na agizo la kuhamishiwa kwa mwajiri mwingine.
Vibarua hao zaidi ya 160 wanaojenga barabara za mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam, kwa kushirikiana na wafanyakazi waliojiriwa waligoma na kufunga lango kuu la kuingia ofisi za kampuni hiyo zilizopo Ubungo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wafanyakazi hao wakiwa katika makundi nje ya lango kuu la kampuni hiyo, huku magari kadhaa yakiwa yamepanga foleni kusubiri kuingia kushusha vifaa.
Wafanyakazi hao walisema wamefikia hatua hiyo kutokana na taarifa za Kampuni ya Raba kuchukua dhamana ya kuwasimamia vibarua wote, hivyo hakutakuwapo na mkataba mwingine kati yao na Strabag. Walisema hatua hiyo ambayo inaonekana kufanyika bila kuzingatia sheria,  kwani walipaswa kulipwa haki zao kabla ya kuhamishiwa kampuni nyingine.
Licha ya madai hayo,  wafanyakazi hao walionekana kulalamikia ujira mdogo  wanaolipwa na Kampuni ya Raba, ikilinganishwa na kiwango walichokuwa wakilipwa na Strabag.
 Walisema  awali walikuwa wakilipwa Sh17,000 kwa siku, lakini baada ya kuhamishwa malipo  yameshuka hadi Sh10,000  ambazo hakiwawezeshi kukidhi mahitaji.
Kufuatia mgomo huo, kuchukua saa kadhaa,  Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana  aliwasili  eneo kuwasikiliza wafanyakazi hao na kupata suluhu.
Rugimbana aliwataka wafanyakazi na vibarua hao wakutane leo kwa ajili ya kutafuta mwafaka.

Wagonjwa wa dengue wafikia 376



Dar es Salaam. Homa ya dengue inaendelea kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari hadi juzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu 376 wamekwishagundulika kuugua ugonjwa huo.
Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa wizara hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema hadi jana watu wawili walikuwa wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema inaweza kuwa kubwa zaidi endapo upimaji utafanyika katika kila wilaya. “Pengine idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu wengi hawapimwi, Ijumaa (kesho) tutatoa, taarifa zaidi,” alisema.
Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa wengi zaidi, ikifuatiwa na Ilala na Temeke. Hata hivyo, alisema huenda wilaya zenye idadi ndogo ya wagonjwa hazijaweza kupima na kubaini watu wenye maradhi hayo ikilinganishwa na Kinondoni.
Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema hali ni mbaya na wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtafiti wa malaria, tabia za mbu na mazingira, wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Nicholas Govela alisema tayari wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa kina kuwajua mbu wanaoeneza homa ya dengue nchini. “Utafiti huu utasaidia kujua ni mbu kiasi gani wameathirika na virusi hivyo. Tukifanya hivyo tutajua ukubwa wa tatizo, tutajua wanapatikana wapi zaidi na virusi vyao vimetokea wapi,” alisema.
Dk Govela alisema ni lazima utafiti huo ufanyike ili kudhibiti maambukizi zaidi ya homa hiyo akisema zipo sababu kadhaa zinazohisiwa kusababisha maradhi hayo, ikiwamo ya wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kuambukizwa kwa njia ya kuumwa na mbu.
“Ugonjwa huu umeenea zaidi nchi za Amerika ya Kusini na Kusini mwa Bara la Asia. Hapa kwetu mbu hawa walikuwapo lakini ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa kiasi hiki, ndiyo maana sababu zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji,” alisema.
Alisema maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mtu mwenye ugonjwa huo kuumwa na mbu hao aina ya Aedes Egyptiae na mbu hao wakichukua virusi, huvisambaza kwa watu wengine. “Inawezekana tatizo ni kubwa zaidi ya hivi inavyofikiriwa kwa sababu wanaokuja hospitali kupimwa na kugundulika ni wachache, wengi wasiofika hawawezi kujulikana,” alisema.
Makazi duni hatarini zaidi
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue, Mrisho Rupinda alisema watu wanaoishi katika makazi duni wapo hatarini kuathiriwa zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa taka nyingi na madimbwi.
Alitoa mfano wa wagonjwa wa kwanza wilayani Kinondoni, akisema walitokea maeneo ya Kambangwa, Mwananyamala Komakoma ambako kulikuwa na madimbwi na bwawa la maji.
“Wagonjwa wengi huonekana zaidi kwenye makazi duni kwa sababu ya mpangilio mbovu na kuzagaa kwa taka. Lakini pia maeneo mengine ambayo watu huhifadhi maji kwenye matenki au ndoo kwa muda mrefu bila kuyafunika,” alisema.